Abstract:
Makala hii inajadili changamoto mbalimbali zinazohusiana na sera
ya lugha. Kwa muda mrefu, nchi ya Tanzania haina sera mahususi ya
lugha, badala yake, masuala ya lugha yameingizwa katika Sera ya
Utamaduni na Sera ya Elimu. Sera ya lugha ni jumla ya mawazo,
matamko, sheria, kanuni na taratibu zenye kufafanua utekelezaji wa
mabadiliko ya matumizi ya lugha (Mekacha, 2000; na Msanjila,
2009). Aidha, makala inafafanua kuhusu dhana, aina ya sera za
lugha, na kuonesha namna sera ya lugha kama ilivyoingizwa katika
Sera ya Utamaduni na Elimu. Data katika makala hii, kwa kiasi
kikubwa, zimekusanywa kutoka maktaba na kwa wadau mbalimbali
wa lugha. Changamoto zilizojadiliwa ni pamoja na: kutokuainishwa
kwa mpango wa utekelezaji wa sera, sera ya lugha kushughulikia
suala la elimu tu, na kutokupewa nafasi ya lugha nyingine za jamii.
Mintarafu ya changamoto hizo, makala imebainisha sababu za
changamoto hizo. Pia, imebainisha umuhimu kuhusu haja ya kuwa na
sera madhubuti na mahususi ya lugha nchini Tanzania.